NIMEAMUA kujiuzulu NAFASI yangu ya Ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama
Cha Mapinduzi CCM, pamoja na nafasi zote za Uongozi ndani ya Chama
kuanzia leo, Oktoba 30, 2017.
HALIKADHALIKA, asubuhi ya leo nimemwandikia Spika wa Bunge, Mh. Job
Ndugai, Mb., barua ya kujiuzulu nafasi yangu ya UBUNGE wa Jimbo la
Singida Kaskazini kupitia tiketi ya CCM, nafasi ambayo nimeitumikia kwa
vipindi vinne mfululizo tangu nilipochaguliwa kwa mara ya kwanza mnamo
mwaka 2000 hadi Sasa.
AIDHA, Nimechukua UAMZI huo kutokana na kutorishwa kwangu na mwenendo
wa hali ya Kisiasa nchini, ikiwa ni pamoja na ukiukwaji wa HAKI za
Kibinadamu, ongezeko la vitendo vya dhuluma wanavyofanyiwa baadhi ya
watanzania wenzetu, na kutokuwepo kwa mipaka ya wazi kati ya MIHIMILI ya
dola (Serikali, Bunge, na Mahakama) kunakofanya utendaji kazi wa
Kibunge wa Kutunga Sheria na wa Kuisimamia Serikali kutokuwa na uhuru
uliainishwa na kuwekwa bayana KIKATIBA.
VILEVILE, Naamini kwamba bila Tanzania kupata Katiba Mpya Sasa,
hakuna namna yeyote ya kuifanya mihimili ya dola isiingiliane na kuwepo
kwa ukomo wa wazi na kujitegemea kwa dhahiri kwa mihimili ya Serikali,
Bunge na mahakama ambayo ndio chimbuko la Uongozi Bora wa nchi, na
kuonesha kwa uwazi kuwa madaraka yote yatokana na wananchi wenyewe, na
kwamba Serikali ni ya Watu kwajili ya Watu.
MIMI Naondoka na kukiacha Chama Cha Mapinduzi CCM, nikiwa
nimekitumikia kuanzia ngazi ya Uenyekiti wa UVCCM Mkoa, Ujumbe wa Kamati
za Siasa Wilaya na Mkoa, Ujumbe wa Kamati ya Wabunge Wote wa CCM na
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM TAIFA, kwani nimejiridhisha kuwa kwa
mwenendo wa hali ya kisiasa, kiuongozi na kiuchumi uliyopo Tanzania
Sasa, CCM imepoteza mwelekeo wake wa kuisimamia Serikali kama ilivyokuwa
hapo awali.
AIDHA, Naamini kuwa, kama ilivyotokea kwa mihimili ya Bunge na
Mahakama kutokuwa na uhuru kamili, bila kuingiliwa kiutendaji kwa namna
Moja au nyigine, CCM nayo imekuwa Chini ya miguu ya dola badala ya chama
kushika hatamu na kuikosoa Serikali inapobidi kama yalivyokuwa maono ya
Baba wa TAIFA MWALIMU Julius Kambarage Nyerere.
HIVYOBASI, kwa dhamira yangu, na kwa uamuzi wangu mwenyewe, nikiwa na
haki ya KIKATIBA, natangaza KUKIHAMA Chama Cha Mapinduzi CCM leo hii,
na nitaomba IKIWAPENDEZA wanachama wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo
CHADEMA, basi waniruhusu kuingia MALANGONI mwao, niwe mwanachama, ili
kuungana na CHADEMA na watanzania wote wanaopenda kuleta mabadiliko ya
kisiasa na kiuchumi nchini kwa kupitia mfumo wa ki demokrasia na uhuru
wa mawazo.
VILEVILE, nimemua kujiuzulu KITI Cha Ubunge, Jimbo la Singida
Kaskazini kuruhusu kufanyika kwa UCHAGUZI mwingine ili wananchi wapate
fursa ya kuchagua ITIKADI wanayoona inawafaa kwa majira na nyakati hizi
zenye changamoto lukuki nchini Tanzania. Ni imani yangu, kamwe
hayatakuwa ya bure maneno haya, wala uamuzi huu niufanyao mbele ya
Watanzania leo ili kwamba, SOTE kama TAIFA tuingie kwenye mjadala wa
kuijenga upya misingi ya nchi yetu.
Ni maombi yangu kwa MUNGU kuwa Haki itamalaki Tanzania. Upendo, amani
na mshikamano wa watu wa imani zote za dini, mitazamo yote ya kiitikadi
za Kisiasa, na makabila yote nchini uimarike. Tushindane ki sera na
kuruhusu tofauti za mawazo, lakini tubaki kama ndugu, na TAIFA lililo
imara na nchi yenye ADILI.
#MunguIbarikiTanzania.
Lazaro S. Nyalandu.
0 comments:
Post a Comment